Rais Buhari: Mke wangu ni wa kwangu jikoni

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amejibu onyo kutoka kwa mkewe ambaye alikuwa ametahadharisha kwamba hatamuunga mkono uchaguzi mkuu ujao iwapo hatafanya mabadiliko serikali.
Bi Aisha, kwenye mahojiano na BBC, alikuwa amedokeza kwamba mumewe amepoteza udhibiti wa serikali.
Bw Buhari kwa sasa yumo kwenye ziara rasmi nchini Ujerumani na kwa mujibu wa shirika la habari la AP, amemjibu mkewe wakati wa kikao cha wanahabari akiwa pamoja na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.
Bw Buhari anaanza kwa kucheka kidogo kisha kusema: "Sijui mke wangu ni wa chama gani, lakini najua yeye ni wa kwangu jikoni na sebuleni na chumba hicho kingine."
Kiongozi huyo aliyeingia madarakani mwaka jana amesema pia kwamba na ujuzi na uzoefu zaidi ya mkewe katika siasa.
Amesema alijaribu kwa miaka 12 kuwa rais na akafanikiwa kwa mara ya nne.
"Kwa hivyo, nina ujuzi kushinda yeye na watu wengine wa upinzani, kwa sababu mwishowe nilifanikiwa. Si rahisi kuridhisha vyama vyote vya upinzani nchini Nigeria au kushiriki serikalini."
Bi Merkel alionekana kushangazwa na matamshi ya Bw Buhari.

             Je Aisha Buhari ni nani?


Alizaliwa mnamo tarehe 17 mwezi wa Februari 1971 Kaskazini mashariki mwa Nigeria katika jimbo la Adamawa.
Aisha Buhari ni mjukuu wa waziri wa kwanza wa ulinzi nchini Nigeria Alhaji Muhammadu Ribadu.
Aliolewa na Muhammadu Buhari mwaka 1989.Wana watoto watano ,mvulana mmoja na wasichana wanne.
Mwaka 1995,alifungua jumba la Hanzy Spa,kaskazi mwa Nigeria ikiwa ndio jumba la kwanza la urembo ,huko Kaduna baada ya kufanikiwa kupata cheti cha Diploma ya urembo kutoka chuo kikuu cha Carlton nchini Uingereza.
Alichapisha kitabu ''Essential of Beauty Therapy'': Kielelezo kamili cha utaalam wa urembo 2014.
Ni wakili wa maswala ya haki za kibinaadamu na amefadhili fedha kuzisaidia familia za waathiriwa wa Boko Haram baada ya zaidi ya wasichana 250 kutekwa na wapiganaji hao 2014.
Aliwashangaza wengi mwaka uliopita baada ya kuonekana hadharani akiwa amevaa saa ya bei ghali,na kuwafanya baadhi ya raia kujiuliza iwapo alikuwa anakandamiza mpango wa rais Buhari kuonekana mtu wa watu.
Bi Buhari pia alikosolewa katika mitandao ya kijamiii kwa kujaribu kusalimiana kwa mkono na Alaafin of Oyo,Chifu wa watu wa Yoruba.
Previous
Next Post »

Ads