Mtanzania wa kwanza kushiriki fainali ya mashindano ya upishi ‘World Food Championship’ Marekani

Mtanzania ‘Chef’ Fred Uisso amechaguliwa kushiriki kwenye fainali za mashindano ya World Food Championships 2016 zinazotarajiwa kufanyika Novemba 8-15, baada ya kufanya vizuri katika upishi wa nyama ‘Best Stake Chef’ mapema mwaka huu.

Chef Uisso ambaye ni mpishi mwandamizi katika mgahawa wa Afrikand uliopo Kinondoni, anakuwa Mwafrika wa kwanza kupata nafasi ya kushiriki katika mashindano hayo, ambayo yamefanyika kwa kipindi cha miaka 15 mfululizo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001 baada ya kufadhiliwa na Red Gold Tanzania.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Chef Uisso alisema amepata nafasi ya kwenda kushiriki mashindano hayo mwezi ujao Alabama States nchini Marekani baada ya kushiriki kupitia mtandaoni mara kadhaa.
“Walinitambua kupitia kazi zangu ambazo nilizifanya mtandaoni, katika dunia nzima ambao tuliingia katika mtandao huo tulikuwa zaidi ya watu 3700 ambao kila mmoja alionyesha uwezo wake wa kupika vyakula mbalimbali, nilirekodi na kuweka katika mtandao huo na majaji watatuchagua washindi 100 katika kila kipengere,” alisema Chef Uisso ambaye ni balozi wa Red Gold Tanzania.
Alisema baada ya kuchaguliwa 100 katika vipengere 9, jumla ya washiriki 900 walipatikana na kuchujwa hadi kufikia 50. Baadaye walipewa kazi nyingine na kisha kuchujwa mpaka kufikia 21 ambao ndiyo walioingia fainali.
“Tumepatikana 21, kati yao 14 ni kutoka katika majimbo mbalimbali nchini Marekani, saba wametoka katika nchi mbalimbali nje ya Marekani na mimi pekee ninawakilisha Afrika kwa hiyo ninaiwakilisha pia nchi yangu Tanzania,” alisema Chef Uisso.
Kuhusu Chef Uisso
Nilivutiwa na kazi hii mwaka 1979 mara baada ya kuajiriwa Mikumi Wildlife Lodge iliyopo ndani ya mbuza za wanyama Mikumi kama Msaidizi wa Utawala. Hoteli ilikuwa chini ya usimamizi wa Hallmark Hotels International.
Niliamua kuanza kujifunza na nilipata mafunzo ya ndani kwa kuwa awali sikuwa katika taaluma ya upishi hasa jikoni na katika migahawa. Lengo lilikuwa ni kuondoa uhaba wa wafanyakazi kwani ilikuwa vigumu kupata watu maeneo ya karibu na Mikumi.
Nilikuwa miongoni mwa watu waliopata ujuzi kwa kipindi cha miaka miwili na baadaye nilihitimu na kuwa mpishi mwandamizi. Nilipoondoka Mikumi Wildlife Lodge mwaka 1980, niliendelea na kazi ya taaluma yangu ya awali kama Meneja Biashara wa makampuni mbalimbali mpaka mwaka 1987 nilipokwenda nchini Uingereza kwa ajili ya masomo ya ‘Development Studies in business management’ yaani maendeleo katika usimamizi wa biashara.
Niliutumia muda wangu wa mapumziko kufanya kazi katika hoteli mbalimbali na migahawa mbalimbali. Hapo nilijifunza zaidi kupika mapishi mbalimbali mapya na ya watu wa mataifa mbalimbali na kujifunza siri zaidi za upishi.
Taratibu wazo la kuwa na mgahawa wangu likaanza kupenya kwenye kichwa changu. Nilianza kwenda kula vyakula katika migahawa na hoteli tofauti ikiwa ni moja ya tafiti zangu, ingawaje zingine zilikuwa ni ghali sana.
Nilirudi nchini kwangu Tanzania niliendelea kufanya kazi kama meneja wa biashara wakati huohuo nikiangalia namna gani nitaanzisha mgahawa wangu. Mwaka 1999 niliamua kununua kipande cha ardhi kwa ajili ya kujenga mgahawa wnagu mwenyewe niliouita “Club Afrikando.”
Nilifungua biashara yangu mwaka 2003 na kuachana na kazi nyingine na nikawekeza nguvu zangu katika biashara yangu kama mpishi mwandamizi na Mkurugenzi Mtendaji wa Club Afrikando.
Leo hii Afikando ni mgahawa unaojulikana zaidi na wengi wanapenda kula vyakula vyangu na ni miongoni mwa migahawa maarufu jijini. Club ni maarufu kwa kutengeneza vyakula mbalimbali vikiwemo Mexican dishes, Cajun, Creole, Oriental, Italian, French, Continental na vyakula mbalimbali vya Kiafrika.
Tuna vyakula aina mbili ambavyo huwezi kuvipata sehemu yoyote ile duniani kama “Afrikando Chips” na chakula kingine ni supu ya kuku ijulikanayo kama “Afrikando Chungu”. Tunapatikana kupitia mtandao wa Instagram kupitia akaunti ya “clubafrikando”.
Malengo yangu ni kumiliki chuo cha upishi ambapo kwa sasa nipo katika mchakato wa awali na natarajia kukifungua mwishoni mwa mwaka huu. Tayari nina wanafunzi 200 wanaosubiri chuo kifunguliwe.
Pili ninamatarajio ya kuwa mpishi mwandamizi maarufu duniani na kushiriki mashindano haya ni moja ya mwanga wa ndoto zangu
Previous
Next Post »

Ads