Dk. Shein aongoza kikao cha wizara ya afya


WIZARA ya Afya imeeleza miongoni mwa juhudi zake inazoendelea kuzichukua katika kuhakikisha sekta hiyo inaimarika ni pamoja na kuwapeleka wataalamu wake wa fani mbali mbali masomoni ili kuendelea kujenga uwezo na kuelekea kwenye kujitegemea.
Hayo yameelezwa na uongozi wa Wizara hiyo, huko Ikulu mjini Zanzibar katika kikao maalum kati ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na uongozi wa Wizara hiyo ilipokuwa ikiwasilisha Taarifa yake ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Wizara kwa kipindi cha Julai hadi Septemba katika Bajeti ya mwaka 2016-2017.
Katika maelezo yake, Waziri wa Wizara hiyo Mahmod Thabit Kombo alisema kuwa Wizara bado inaendelea kupata mafanikio makubwa katika kuendeleza miundombinu yake hasa katika hospitali mpya ya Abdalla Mzee na kuweka vifaa vipya na vya maabara.
Aidha, upanuzi wa hospitali ya Mnazi Mmoja katika wodi ya watoto na kina mama pamoja na kuweka vifaa vipya na vya kisasa katika jengo hilo jipya.
Pia, hospitali ya Kivunge imeendelea kuimarishwa kwa kujenga jengo jipya la wagonjwa wa nje pamoja na ukarabati wa maabara.
Waziri Kombo alitumia fursa hiyo kueleza majukumu Makuu ya Wizara hiyo ambapo pamoja na majukumu hayo Wizara imezingatia Sera, Mipango na mikakari mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa ikiwa ni pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030, Dira ya Zanzibar 2020, Sera ya Afya 2011, Mpango Mkakati wa III wa Sekta ya Afya pamoja na Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwak 2015-2020.
Uongozi huo pia, ulizipongeza juhudi za Dk. Shein anazozichukua katika kuwapa maelekezo na ushauri ambao unaendelea kuwasaidia katika utendaji wao wa kazi.
Katika suala zima la upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya, uongozi huo umezipongeza juhudi zilizochukuliwa na Serikali katika kuhakisha Bohari yake kuu inazo dawa za kutosha.
Uongozi huo pia, ulieleza juhudi za makusudi zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara hiyo katika uanzishwaji wa Bima ya Afya pamoja na hatua zilizofikiwa.
Mapema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alizipongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara hiyo katika utoaji huduma ya afya kwa wananchi hapa nchini.
Dk. Shein alieleza haja ya kuendelea na utaratibu wa kuwapa mafunzo watendaji wa Wizara hiyo katika kada mbali mbali kwa lengo la kuja kutoa huduma kwa wananchi huku akisisitiza azma ya Serikali kupitia Wizara hiyo kuendelea kutoa huduma mbali mbali za upasuaji ambazo zitapunguza gharama za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kulipa kipaumbele suala zima la utafiti ndani ya Wizara hiyo huku akisisitiza suala zima la uzalendo na kueleza kuwa utaratibu wa kuwapeleka watendaji wa Serikali kufanya kazi Pemba sio adhabu bali ni taratibu za kiutumishi.
Nae Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Abdulhamid Yahya Mzee, aliipongeza Wizara hiyo kwa kuwasilisha vyema Mpango Kazi wake huku akisisitiza umhimu wa mikutano hiyo kwa manufaa ya Serikali sambamba na upangaji mzuri wa huduma za maendeleo endelevu.
Previous
Next Post »

Ads