Kundi la wachunguzi wa kimataifa waliochunguza kutunguliwa kwa ndege ya shirika la Malaysia Airlines


Kundi la wachunguzi wa kimataifa waliochunguza kutunguliwa kwa ndege ya shirika la Malaysia Airlines safari nambari MH17, linatarajiwa kutoa ripoti ya matokeo ya uchunguzi leo Jumatano.
Ndege hiyo ilitunguliwa ilipokuwa katika anga ya mashariki mwa Ukraine mwaka 2014.
Watu wote 298 waliokuwa kwenye ndege hiyo aina ya Boeing 777 iliyokuwa safarini kutoka Amsterdam kuelekea Kuala Lumpur walifariki baada ya ndege hiyo kuanguka eneo la Grabovo jimbo la Donetsk .
Uchunguzi wa awali ulioongozwa na Bodi ya Usalama ya Uholanzi ulisema kombora aina ya Buk lililoundiwa Urusi lilitumiwa kutungua ndege hiyo.
Sasa, kundi la wachunguzi wa kimataifa wanaoongozwa na wataalamu kutoka Uholanzi, linatarajiwa kueleza hasa kombora lilitoka wapi.
Maafisa wa mashtaka kutoka Australia, Ubelgiji, Malaysia na Ukraine pia walishiriki katika uchunguzi huo.
Nani wa kulaumiwa?
Waasi walioungwa mkono na Urusi walilaumiwa na Ukraine na nchi za Magharibi na kudaiwa kutungua ndege hiyo 17 Julai 2014.
Wakati huo, wanajeshi wa Ukraine walikuwa kwenye vita vikali na waasi hao waliotaka kujitenga kwa maeneo ya mashariki mwa Ukraine.
Urusi imekana kuhusika na pia kupuuzilia mbali madai kwamba mtambo uliorusha kombora hilo la Buk ulikuwa maeneo ya Urusi.
Lakini baada ya kisa hicho, Umoja wa Ulaya (EU) na Marekani waliiwekea vikwazo Urusi.
Mapema wiki hii, Urusi ilitoa picha za mitambo ya rada, ambazo ilisema zinaonesha ndege hiyo haingetunguliwa na watu kutoka maeneo yaliyoshikiliwa na waasi.
Wakosoaji wa Urusi wanasema Urusi imetoa simulizi tatu tofauti kuhusu matukio yaliyojiri wakati wa kutunguliwa kwa ndege hiyo.
Previous
Next Post »

Ads