Rais Peter Mutharika wa Malawi amevunja kimya chake kuhusu uvumi ulioenea kwa siku kadhaa nchini humo kuwa ameaga dunia na kusema kuwa walioeneza habari hizo wanapaswa kuuzwa.
Saulos Chilima, Makamu wa Rais wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika amesema Rais Mutharika 'hajashangazwa na uvumi huo na kwamba anatarajiwa kurejea nchini kutoka nje ya nchi.
Hata hivyo taarifa ya ofisi ya Makamu wa Rais wa Malawi haijatoa maelezo zaidi kuhusu alikokuwa Mutharika na sababu za yeye kuwa nje ya nchi kwa takriban mwezi mmoja bila maelezo yoyote kwa wananchi.
Rais Mutharika hajaonekana hadharani tangu baada ya kuhutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini New York mwezi Septemba, jambo ambalo lilichangia kusambaa kwa kasi, uvumi kuwa ameaga dunia akitibiwa katika hospitali moja nchini Marekani.
Siku chache zilizopita, Malison Ndau, msemaji wa serikali ya Malawi alisema Rais Mutharika alibakia Marekani baada ya mkutano wa UN, kwa shabaha ya kukutana na kufanya mikutano kadhaa na viongozi mbali mbali wa dunia.
Mashirika ya kijamii kikiwemo Chama cha Mawakili nchini humo, yamekuwa yakikosoa kimya cha serikali kuhusu aliko Rais Mutharika na kusisitiza kuwa, wananchi wana haki ya kikatiba kujua hali ya kiongozi wa taifa.
ConversionConversion EmoticonEmoticon