HISTORIA:Oparesheni Entebbe, Steringi Alifia Uwanja Wa Mapambano

Juni 27, 1976 ndege ya Ufaransa ‘Air France Flight 139’ ikiwa na abiria 248 ndani yake ilitekwa na magaidi  wanne. Ambao walikuwa Wapalestina 2 na Wajerumani 2 baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Athens, Ugiriki.
Air France.
Magaidi wa Kipalestina walitumwa na gaidi hatari Wadie Haddad, aliyekuwa kiongozi wa kundi hatari la kigaidi la Popular Front for the Liberation of Palestine–External Operations (PFLP-EO) wakisaidiwa na wenzao waliokuwa wanachama wa kundi jingine hatari la German Revolutionary Cells.
Makundi yote mawili yalikuwa yakiendesha harakati za kupambana na Waisrael popote pale walipo chini ya jua.
Lengo kuu la kuiteka ndege hiyo ilikuwa kuilazimisha serikali ya Israel kuwaachia wafungwa wa Kipalestina zaidi ya 40 waliofungwa nchini Israel pamoja na wengine 13 waliokuwa wakitumikia kifungo katika nchi mbalimbali.
Air France ilianza safari yake jijini Tel Aviv, Israel kuelekea jijini Paris, Ufaransa na baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Athens, Ugiriki magaidi hao wakiwa na silaha za moto yakiwepo mabomu na bunduki waliwalazimisha marubani kubadili safari ya kuelekea Paris na waelekee Entebbe, Uganda kupitia Uwanja wa Ndege wa Benghazi, Misri.
Juni 29, 1976, baada ya kuwa angani kwa muda wa siku mbili hatimaye Air France Flight 139 ilitua uwanja wa ndege wa Entebbe, Uganda zaidi ya umbali wa kilomita 4,000 kutoka Israel.
Rais Idd Amin aliwaunga mkono magaidi hao na kuwapa jengo la kuwahifadhi abiria wote 248. Alifanya hivyo kwasasababu kubwa moja alikuwa anataka kuungwa mkono na mataifa makubwa ya kiarabu ambayo yalikuwa na ugomvi na Israel. Aliwapa silaha na askari wa kutosha kuhakikisha hakuna abiria anayetoroka.
Rais Idd Amin.
Baada ya siku mbili tangu kuwasili Entebbe abiria wote walitenganishwa kulingana na utaifa wao. Abiria 148 wasio raia wa Israel waliachiwa na wakabaki abiria 94 wenye uraia wa Israel pamoja na marubani na wafanyakazi wengine 12.
Magaidi walitishia kuwaua mateka wote 96 endapo wafungwa wa Kipalestina hawataachiwa.
TEL AVIV, ISRAEL
waziri Mkuu wa Israel  (wakati huo), Yitzhak Rabin alikutana na kufanya kikao cha siri na Mkurugenzi Mkuu wa MOSSAD, Meja Jenerali Yitzhak Hofi. Kikao hicho cha siri kilifanyika kwenye makao makuu ya MOSSAD jijini Tel Aviv.
Yitzhak Rabin.
Ngoja nikueleze jambo moja la muhimu hapa, MOSSAD ni Shirika la Ujasusi la Israel, ni moja ya mashirika ya kijasusi yenye mbinu na ujuzi wa hali ya juu duniani. Wao ndiyo wanahusika na masuala yote nyeti ya kiusalama ya Israel. Wapo wanaoamini MOSSAD ina ujuzi wa juu kuliko hata mashirika ya kijasusi ya CIA (Marekani), M16 (Uingereza) na GRU (Urusi).
Meja Jenerali Yitzhak Hofi (kulia).
Baada ya kikao hicho viongozi hao walikubaliana kupeleka kikosi cha makomando 100 kutoka MOSSAD kwenda kuwakomboa raia wao wakiwa hai na endapo itatokea mmoja wao ameuawa na vikosi vya magaidi basi lazima maiti yake irudi Israel, hawakutaka kuacha kitu Uganda, hawakutaka damu yao ibaki uganda, hawakutaka kumpa Idd Amin kiburi na majigambo.
Meja Jenerali Yitzhak Hofi.
Kikosi maalum cha makomando kiliandaliwa chini ya komando wa vita Luteni Kanali, Yonatan Netanyahu ‘Yoni’, kikosi hiki kilipewa jina la Sayeret Matkal kwa maana ya kikosi cha ukombozi na jina la Oparesheni waliipa Code ya Operation Thunderbolt, maana yake Oparesheni Radi.
… Sehemu ya kikosi cha makomando wa MOSSAD.
Baada ya wiki moja ya maandalizi hatimaye usiku wa Julai 4, 1976 ndege za kijeshi ya Israel zikiwa na makomando 100 ndani yake zilianza safari yake ya kuelekea Entebbe, Uganda.
Ndege hizo za kijeshi aina ya Lockheed C-130 Hercules zilikuwa zikiongozwa na rubani ambaye pia ni Komando mwenye cheo cha Luteni kanali, Joshua Shani, kutokana na umbali wa kilometa zaidi ya 4000 kutoka Israel ililazimika kutafuta nchi moja wapo ya Afrika Mashariki ili waweze kujaza mafuta.
Yitzhak Rabin (katikati) akiwa na baadhi ya makomando.
Ilikuwa ni lazima wajaze mafuta kwasasabu moja kubwa wakati huo ndege zao hazikuwa na uwezo wa kujaza mafuta zikiwa angani. Hivyo ili waweze kwenda na kurudi Entebbe ilikuwa ni lazima wajaze mafuta kabla ya kuwasili Entebbe. Swali likawa wapi watajaza mafuta? kila nchi ilikuwa inamuogopa Idd Amin, hakuna nchi iliyotaka kuingia kwenye mgogoro na dikteta huyu aliyekuwa na vitisho vya kila aina.
Baada ya majadiliano ya muda mrefu Waziri wa Kilimo wa Kenya Bruce MacKenzie alienda ikulu kumuomba Rais Jommo Kenyatta akubali ndege hizo za kijeshi zitue na kujaza mafuta Airspace ambapo leo ndiyo Jommo Kenyatta International Airport.
Ombi hilo lilifanikiwa na MOSSAD walifanya maandalizi yote ya mwisho kutoka Airspace (Jommo Kenyatta International Airport) kwa msaada mkubwa wa MacKenzie ambaye baadaye alikuja kuuawa na vikosi vya Amin.
Julai 4,1976 ndege kubwa ya kijeshi ya Israel, Air Force C-130 ililianza safari ya kuelekea Entebbe. Usiku huu uliobatizwa jina la Oparesheni Radi. Ilielekea Uwanja wa ndege wa Entebbe bila kuonekana kwenye rada za kuongozea ndege. Hapa ndipo uelewe MOSSAD ni majasusi wa hali ya juu.
JINSI ILIVYOKUWA
Ndege hizi za kijeshi zilitoka Israel na kupaa umbali wa mita 30 tu kutoka usawa wa bahari lengo likiwa kukwepa kuonekana kwenye rada za kuongozea ndege kwenye nchi za Misri, Sudan na Saudi Arabia waliokuwa marafiki wa karibu wa Idd Amni.
Baada ya safari ndefu ndege moja kubwa ilitua Nairobi na nyingine ilishika uelekeo wa Entebbe.
Boeing 707 iliyotua Uwanja wa Ndege wa Jommo Kenyatta ilikuwa na madawa ya tiba ya binadamu na nyingine iliyokuwa imebeba makomando ilitua Uwanja wa Ndege wa Entebbe.
Makomando hao waliwasili Entebbe Julai 3 saa tano kamili usiku, wakiwa na ndege hiyo ya kijeshi ya kubebea mizigo, mara mlango mkubwa wa ndege hiyo ukafunguliwa na Mercedes nyeusi na Landlover zinazofanana kwa kila kitu na zile alizokuwa akitumia Dikteta Idd Amin kwenye misafara yake zilishuka kutoka kwenye ndege.
Mercedes Benz iliyotumiwa na MOSSAD.
Magari hayo yalielekea moja kwa moja kwenye jengo lililohifadhi mateka hao 106. Jengo hili lilikuwa ndani ya uwanja huo wa Entebbe.
Jambo moja ambalo MOSSAD huenda walidanganywa au walipotoshwa ni kwamba hawakujua siku chache zilizopita Idd Amin alikuwa amenunua Mercedes Benz nyingine yenye rangi nyeupe, hivyo walisimamishwa na walinzi wa uwanja huo wa ndege.
Bila kupoteza muda Makomando wa MOSSAD waliwamiminia risasi walinzi hawa kwa kutumia bastola maalum ambazo hazitoi sauti.
Walifanikiwa kuingia na kuwakomboa mateka 102 kati ya 104, bahati mbaya mateka wanne waliuawa.
Kwenye Oparesheni Radi pia kiongozi mkuu aliyewaongoza makomando kuingia ndani ya uwanja wa ndege na kuongoza mapambano ya kuwaua magaidi wote wa nne na kufanikisha ukombozi huo, Luteni Kanali Yonathan Netanyau naye aliuawa baada ya kupigwa risasi kifuani na walinzi wa Idd Amin. Aliuawa wakati akiwasaidia mateka wengine kuingia ndani ya ndege, aliyeumuua naye aliuawa na makomando wa MOSSAD.
Luteni Kanali Yonathan Netanyau.
Baada ya kuwabeba mateka na maiti hao ndege hiyo iliondoka na kutua jijini Nairobi ambako ndege nyingine ya kijeshi iliyokuwa na madawa ndani yake ilikuwa inawasubiri.
Majeruhi wote walipatiwa tiba na wengine wawili walikimbizwa Hospitali kisha kupaa hadi Tel Aviv na kupokelewa na mamia ya wananchi.
…Mateka baada ya kuwasili Tel Aviv.
Komando Yonathan Netanyau alizikwa kwenye makaburi ya watu na viongozi maarufu yajulikanayo kwa jina la Mount Herzi.
Oparesheni Radi ilibadilishwa jina na kuitwa Mivitsa Jonathan ‘Operation Jonathan’ maana yake Oparesheni Jonathan.
Naam zilikuwa dakika 90 za mapigano makali Uwanja wa Ndege Entebbe, mahali ambako steringi anaongoza mapamabano na kushinda na yeye kuuawa dakika chache kabla ya kuondoka uwanja wa mapambano.
Hivi ndivyo steringi alifia vitani na Dikteta Idd Amin alifichama kabatini baada ya kupigiwa simu kwamba makomando wa Israel wamevamia na kukomboa mateka wote, mbaya zaidi alidanganywa kuwa sasa makomando hao wanaelekea Ikulu, mahali aliko.

                               CREDIT:Leonard Msigwa
Previous
Next Post »

Ads