Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeahirisha mikutano na maandamano ya hadhara ya UKUTA iliyopanga kuifanya kesho nchi nzima na kwamba itatangaza siku na tarehe itakayopangwa baadae kwa kuzingatia hali halisi ya kisiasa itakavyokuwa nchini.
Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Aikael Mbowe amesema kuwa sababu iliyopelekea kuahirisha maandamano hayo kwa sasa, ni kuwa chama hicho kinapanga kutumia mbinu za kidiplomasia pamoja na harakati nyingine ili kufanikisha UKUTA pasipo kuathiri wanachama wake na nchi kiujumla.
“Siku ya jana, Kamati Maalumu ya Kamati Kuu ya chama chetu ilikutana ili kutafakari hali ya kisiasa nchini, kamati imetujulisha kuwa hadi leo viongozi wa dini hawajatupa taarifa zozote kuhusu jitihada zao za kuonana na rais Magufuli, kutokana na hilo, kamati hiyo imeona bora isogeze siku na tarehe nyingine ambayo hatutaitaja kwa sababu taarifa zetu za intelijensia zinaonyesha kuwa kila tukitaja tarehe wenzetu wanapanga njama za kuua watu siku hiyo ili kuwaaminisha watu kuwa UKUTA ndiyo imeua watu,” amesema.
Amesema kufuatia jeshi la polisi kuondoa zuio la mikutano ya ndani, chama hicho kitaitumia fursa hiyo kutekeleza UKUTA pamoja na kukijenga chama hicho.
“Kufuatia kuondolewa kwa zuio haramu la mikutano ya ndani ya vyama vya siasa, kamati maalumu ya Kamati Kuu imeamua kufanya ziara katika Kanda na mikoa ya kichama ili kuendeleza harakati za UKUTA, kujenga na kuimarisha uhai wa chama chetu na UKAWA,” amesema.
Ametaja mbinu nyingine ya kutekeleza UKUTA kuwa ni kuishtaki serikali katika jumuiya za kimataifa pamoja na taasisi zinazoshughulikia masuala ya haki za binadamu duniani.
“Baadhi ya viongozi wetu walifanya ziara nchi za nje ya nchi kuelezea mataifa namna ya uvunjwaji wa haki unavyoendelea nchini, tutakwenda katika nchi za Asia, Amerika, Umoja wa Afrika na taasisi zinazoshuhulika na masuala ya haki za binadamu,” amesema.
Aidha, Mbowe amesema kamati maalumu ya Kamati Kuu ya chama hicho, imeelezwa juu ya maandalizi ya kufungua mashauri mahakamani kupinga hatua alizodai kuwa ni za ukandamizaji wa demokrasia na haki za binadamu pamoja na ukiukwaji wa katiba na sheria za nchi.
ConversionConversion EmoticonEmoticon