Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba leo ametamba kuwa yeye ni mwenyekiti halali wa chama hicho na kwamba hakuna mtu yeyote atakaye mvua wadhifa huo zaidi ya maamuzi ya wajumbe wa mkutano mkuu ambao amedai kuwa asilimia kubwa wana muunga mkono.
Lipumba ameyasema hayo katika ofisi za makao makuu ya CUF yaliyopo Buguruni jijini Dar es Salaam.
Lipumba amesema kuwa yeye bado ni mwenyekiti halali wa CUF Taifa kwa kuwa aliitengua barua ya kujiudhuru kwake kabla ya mkutano mkuu wenye mamlaka ya kukubali barua ya kujidhuru kwake kuketi na kuiridhia.
Pia amesema kikao kilichoketi Zanzibar cha Baraza Kuu la Uongozi CUF kilikuwa batili kwa kuwa hakikufuata utaratibu na kanuni za katiba ya chama hicho. Amefafanua kwamba , katiba ya CUF inasema kuwa mwenye mamlaka ya kuitisha mkutano au kikao cha dharula ni Katibu Mkuu wa Chama hicho na kwamba Maalim Seif Shariff Hamadi mwenye wadhifa huo alikuwa nje ya nchi, hivyo aliyekuwa na mamlaka ya kukaimu wadhifu huo ni Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya ambaye hakupewa taarifa ya kikao hicho na wala hakuitisha kikao cha kamati ya utendaji ambacho kingeidhinisha kufanyika mkutano huo, na wala hakuitisha mkutano huo.
Hata hivyo, Profesa Lipumba amesema katiba ya CUF inasema kuwa mwenyekiti huvuliwa wadhifa wake pale ambapo wajumbe wa mkutano mkuu kutoka Bara na Zanzibar kuridhia kuvuliwa uenyekiti na kwamba hayo hayakufanyika.
“Ukizingatia katiba usingepata theluthi mbili ya wajumbe wa mkutano mkuu ambao wangeikubali barua ya kujiudhuru kwangu, ” amesema.
Katika hatua nyingine Lipumba amesema anatarajia kuteua wakurugenzi wapya siku za hivi karibuni.
“Mamlaka niliyonayo yananiruhusu kuteua wakurugenzi, na hiyo kazi nitaifanya nitakapo imaliza nitawajulisha,” amesema.
Hali kadhalika, Lipumba amesema wabunge, viongozi na wanachama waliovuliwa na au kusimamishwa uanachama watarejea kwenye wadhifa wao kwa kuwa maamuzi ya kusimamishwa na au kufukuzwa kwao yalikuwa batili.
Amemtaka Katibu Mkuu Maalim Seif kushirikiana nae na kumtoa wasisi kuwa akifika katika ofisi hizo hatodhulika na walinzi wa chama hicho kwa kuwa wako kikatiba kulinda mali na viongozi wa chama hicho.
“Asiwe na wasiwasi kwa ajili ya walinzi kwa sababu wako kikatiba, mimi wala sijaenda omba ulinzi polisi na sijawaona hapa, waliokuwepo ni walinzi wa kila siku na anawafahamu, ” amesema.
Ameongeza kuwa “Katibu mkuu afuate katiba yetu, na kwenye siasa watu hutumia hekima kwa sababu mawazo tunatofautiana,”
Kuhusu mgogoro uliokuwepo CUF, amesema atawasilina na Baraza la Wazee waasisi wa CUF ili wamsihi Maalim Seif akubali suluhu ya mgogoro huo.
Amesema CUF itaendelea kuwa imara na haitameguka kama baadhi ya watu wanavyosema na kuwaomba wanzanzibar kutokubali kurubuniwa na kudanganywa kuwa yeye hana uchungu na taifa hilo.
“Matatizo ya Zanzibar yanajulikana yapo kwa muda mrefu, miaka mingi nimekuwa nikitetea masilahi ya wanzanzibar hata siku moja sikuona viongozi wa Chadema wakiwatetea zaidi ya marehemu Bob Chacha Wangwe,” amesema.
ConversionConversion EmoticonEmoticon