Mexico kumkabidhi El Chapo kwa maafisa Marekani

 Kuna mambo yanaumiza sana katika soka la Tanzania: Kwanini Stand United wanashindwa kumthamini mkufunzi bora kama Mfaransa, Patrick Liewig. Nimesikitishwa sana kama kweli kocha huyo ameaondoka Shinyanga na kuja hapa Dar es Salaam.
Ni habari mbaya upande wangu. Watanzania tumebarikiwa amani na majungu kupita kiasi. Tafadhali, Mwadui FC mchukueni kocha huyu awape ubora….
Liewig ameondoka katika timu hiyo, huku habari zilizopo kocha huyo yupo Dar es Salaam. Leo Stand United watakuwa na mchezo katika uwanja wa Kambarage dhidi ya African Lyon lakini hawatakuwa na kocha huyo aliyeisimamia Stand katika michezo 9 pasipo kupoteza msimu huu.
Simpigii debe, lakini ningependa kuona kocha huyu akibaki katika soka la Tanzania. Liewig, Mholland, Hans Van der Pluijm, Mzambia, Patrick Phiri, Mmalawi, Jacky Chamangwana, Mkenya, Tom Olaba na mtu mwenye mafanikio zaidi kiufundishaji katika soka la Tanzania, Mkenya, James Siang’a (Mwenyezi Mungu amrehemu.) Hawa ni makocha bora zaidi wa kigeni ambao nimepata kuwashuhudia katika ‘karne mpya.’
Nilikuwa na matumaini makubwa na Stand chini ya Liewig, niliamini wangepata mafanikio kwa pamoja kutokana na kwamba, kocha huyo ni kama alikula ‘kiapo’ na wachezaji wake.
Nani ambaye aliipa nafasi Stand kuishinda Yanga SC msimu huu? Nani alitegemea timu hiyo ya Liewig ingesawazisha na kufunga magoli mawili pale Mwadui Complex katika sare ya Mwadui 2-2 Stand? Sikutaraji timu hiyo kama ingemaliza dakika 90′ pasipo kuruhusu goli vs Mbeya City FC pale Sokoine Stadium! Nakumbuka baada ya suluhu-tasa vs City, Liewig alisema wazi kwamba wachezaji wake hawajalipwa kwa miezi mitatu!
Lakini bado wachezaji wake walimsikiliza na kupambana kisha kuichapa Azam FC katika mchezo wa tisa wa VPL siku ya Jumatano iliyopita. Haya ndiyo ‘malipo ya dhati ya wachezaji’ kwa kocha wao.
Wakati, Chamangwa, Siang’a, Phiri, Hans walipata mafanikio katika soka la Tanzania wakizitumia timu kubwa za Yanga na Simba, Liewig aliamua kuwaacha mastaa kama Amri Maftah, Juma Nyosso, Felix Sunzu, Haruna Moshi ‘Boban,’ Mwinyi Kazimoto, na kuwapa nafasi vijana kama Jonas Mkude, William Lucian, Abdallah Seseme, na kuwafanya wacheze katika kiwango cha juu vs Yanga siku ya mwisho ya msimu wa 2012/13.
Hapo ndipo nilipo jenga imani yangu kwake. Wakati mwingine makocha huangushwa na tabia mbaya za wachezaji, lakini tayari Mfaransa huyu alishajitengenezea taratibu zake na jinsi ya kutengeneza timu bora.
Rejea miezi yake mitano kama kocha wa Simba, aliwafanya vijana wacheze kwa ajili ya timu na si watu.
Timu ilikuwa ikicheza kwa nidhamu, na baada ya kutua Stand msimu uliopita amewekeza pia jambo hilo ndio maana watovu wote wa nidhamu waliondolewa katika timu.
Nakosa cha kusema, litakapotoka tangazo rasmi la Stand kuachana na Liewig nitakuwa na mengi ya kusema. Sehemu ya moyo wangu itasononeka sana ikitokea Liewig akaondoka katika soka la Tanzania.
Mtu mvumilivu huyu, mtaalam wa ufundishaji ambaye huwajenga wachezaji na kuwasisitiza kucheza kwa ajili ya timu. ‘Kwanini Stand United inamuacha Patrick Liewig?
Previous
Next Post »

Ads