WAZIRI MKUU ATAKA ORODHA YA WADAIWA SUGU DUWASA


Waziri mkuu akiwasalimia wananchi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza apatiwe orodha ya wadaiwa sugu wa taasisi zote za Serikali mkoani Dodoma ambao wamelimbikiza deni la sh. bilioni 1.4 zikiwa ni bili zao za maji.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Oktoba 2, 2016) wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dodoma (DUWASA) mara baada ya kukagua utendaji kazi wa chanzo cha maji cha Mzakwe nje kidogo ya mji wa Dodoma.

“Niletee haraka orodha ya wadaiwa wote wa Ofisi za Serikali na taasisi za umma ambao hawajalipa bili zao. Madeni yote ni lazima yalipwe,” amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu ambaye yuko katika ziara ya siku mbili ya kukagua maandalizi ya Serikali kuhamia Dodoma, anatembelea sehemu mbalimbali za kutolea huduma za jamii pamoja na kukagua miundombinu ya mkoa huo.

Aliutaka uongozi wa DUWASA na watumishi wote wahakakishe wanaboresha huduma za upatikanaji wa maji hasa kwenye maeneo yanayopimwa viwanja ili wananchi au wawekezaji wanaponunua viwanja wakute huduma hiyo ipo na waanze ujenzi mara moja.

“Tumealika wawekezaji, nataka wajenge viwanda na mahoteli hapa Dodoma, sasa wakikuta maji na umeme kwenye maeneo yao, itakuwa ni kichocheo cha kuharakisha kazi za ujenzi,” amesema.

Pia amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Bi. Christina Mndeme ahakikishe eneo lililo jirani na chanzo hicho cha maji halikaliwi na mtu yeyote na linalindwa dhidi ya uchomaji mioto.

“Uchomaji moto uoto wa asili umeharibu vyanzo vingi vya maji. Ni tatizo kubwa hapa nchini na halina budi kusimamiwa hadi liishe,” amesisistiza.

Amefikia uamuzi huo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi David Pallangyo kwamba kuna wananchi wameanza kujenga na kufanya shughuli za kijamii jirani na chanzo hicho licha ya kuwa walikwishaondolewa zamani.

Kuhusu wadaiwa sugu, Mhandisi Pallangyo alisema mashirika ya umma na taasisi za Serikali ndiyo wanaongoza kwa kulimbikiza madeni. “Wananchi wa kawaida wapo wanaodaiwa lakini deni lao siyo kubwa na hao tunawamudu,” alisema wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi.

Alisema changamoto nyingine inayowakabili ni uchomaji moto ambapo hivi karibuni uliwashwa moto na kuunguza baadhi ya nguzo za umeme ambazo zinapeleka umeme kwenye chanzo hicho.

Alisema askari wa JKT Makutupora walisaidia kuzima moto huo ili usifike kwenye mitambo mingine ya chanzo hicho cha maji
Pia waziri mkuuKassim Majaliwa amewataka watumishi wa afya nchini kufanya kazi kwakuzingatia maadili ya kazi ya utumishi wa umma,kuwa waaminifu ikiwa ni pamoja na kushirikiana.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo leo mjini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa afya wakiwemo wauguzi na madaktari wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma mara alipofanya ziara yake katika maeneo mbalimbali ya mji huo.

Amebainisha kuwa ni vyema watumishi wa afya nchini wakazingatia maadili ya kazi zao kwa kuwa waadilifu na waaminifu ili kuweza kuondoa malalamiko kwa wananchi.

Aidha amewataka wawekezaji kujitokeza kujenga hospitali katika mji wa Dodoma kutokana na ujio wa Serikali kuhamia Dodoma katika kukidhi huduma ya matibabu.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Dk.James Charles  amesema kuwa hospitali hiyo imekuwa ikiwahudumia wakazi wengi wakiwemo wa mikoa ya Singida na Iringa hivyo ni vyema Serikali ikaipandisha hadhi hospitali hiyo.
Mganga mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Dk.James Charles

    Katika hatua nyingine Waziri Mkuu ameliagiza baraza la madiwani la Manispaa ya Dodoma kupitia upya suala la kodi ya soko kwa wafanyabiashara wa soko kuu la Majengo ili kuwapunguzia gharama ya kodi.

Naye Mwenyekiti wa Soko kuu la Majengo,Godson Rugazama amesema kuwa sekta ya masoko katika mkoa wa Dodoma imesahaulika hususani katika soko hilo ambapo miundombinu yake imechakaa.
Previous
Next Post »

Ads